Tuesday, October 15, 2013

Risala ya Mhe:Rais wa Zanzibar na MBLM,kwa ajili ya uzinduzi wa sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi.


Ndugu Wananchi,
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mara nyengine kwa kutujaalia kufunga na kukamilisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na tukaweza kusherehekea Sikukuu ya Idd el Fitri kwa furaha, amani na utulivu. Namuomba Mwenyezi Mungu (SW) azikubali ibada zetu na atuzidishie amani, utulivu na kila lenye kheri katika nchi yetu. Kama tunavyoelewa, kila ifikapo tarehe 12 Januari ya kila mwaka, nchi yetuhuadhimisha Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.Mapinduzi haya ambayo yaliongozwa na Jemedari wetu Mkuu, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ndiyo yaliyowakomboa wananchi wa Zanzibar kwa kuondoa utawala wa kigeni, ubaguzi wa watu na kuweka usawa katika jamii ya Wazanzibari. Hivyo, ni wazi kuwa Mapinduzi haya ndiyo msingi wa uhuru, usawa na maendeleo katika nchi yetu hadi tulipofikia.

Miezi mitano ijayo, yaani ifikapo tarehe 12 Januari, 2014, Mapinduzi yetu yatakuwa yamefikia miaka 50 sawa na nusu karne. Bila ya shaka, nusu karne hii ya Mapinduzi inatufikia wakati nchi yetu ikiwa imepiga hatua kubwa za kimaendeleo na kuimarika kwa hali ya amani, utulivu, umoja na mshikamano. Kutokana na hali hiyo, ni dhahiri kuwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuadhimisha kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi yetu kwa sherehe za aina yake, zenye hadhi na haiba inayolingana na mafanikio ya maendeleo tuliyofikia.

Ndugu Wananchi,
Sherehe zetu hizi zinakwenda na kauli mbiu isemayo “Tuimarishe Amani, Umoja na Maendeleo – Mapinduzi Daima”. Kauli mbiu hii inatushajiisha wananchi wote
kujivunia Amani tuliyonayo, Umoja tulionao na hatua kubwa ya Maendeleo tuliyofikia. Jambo la msingi kabisa ni kuilinda amani hiyo, kudumisha umoja wetu na pia kuthamini, kuyaenzi na kuyaimarisha maendeleo yetu. Ni vyema tukatambua kuwa mambo hayo ndiyo hazina muhimu kwa mustakbali mwema wa Wazanzibari na Watanzania wote tuliopo na wale watakaokuja baada ya sisi.
Ndugu Wananchi,
Katika kuadhimisha Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi yetu Matukufu, Serikali imepanga kufanya mambo mbali mbali katika kipindi hiki cha miezi mitano kabla ya kufikia kilele hapo tarehe 12 Januari, 2014 katika Uwanja wa Amaan. Serikali imetoa muongozo wa namna sherehe hizi zitakavyofanyika katika maeneo mbali mbali ya visiwa vyetu vya Unguja na Pemba kwa shamra shamra na mvuto wa kipekee. Bila ya shaka, sote tuna wajibu wa kufuata maelekezo yaliyomo katika muongozo huo na yale yatakayokuwa yanatolewa na viongozi wetu kila mara ili sherehe zetu zifanyike kwa utaratibu maalum wenye kupendeza na usiokuwa na bughudha.
Ndugu Wananchi,
Ni vyema tukaelewa kuwa sherehe hizi ni za kila mmoja wetu, si za Serikali peke yake wala si za chama fulani; ni za kila mwananchi awe mmoja mmoja au kwa makundi. Kila mtu ana wajibu na haki ya kushiriki katika shamra shamra za sherehe hizi kwa namna utaratibu utakavyoelekeza.

Ni dhahiri kuwa matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya kipindi hiki cha miaka 50 yanabainika waziwazi katika kila sekta na nyanja za maisha yetu iwe ni serikalini au ndani ya jamii katika maeneo tunamoishi. Tunapaswa kujivunia na kuyathamini mafanikio hayo ya Mapinduzi nchini kwa vitendo. Hatua kubwa ya maendeleo tuliyofikia ni ithibati na kielelezo muhimu cha ufanisi kwa wale wote wanaoikumbuka
Zanzibar ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964. Sote tuna jukumu la kuyaimarisha maendeleo hayo na kudumisha hali ya amani na umoja wetu. Napenda kutoa wito kwenu wananchi nyote, taasisi za serikali ambazo tayari
zimeshaelekezwa, taasisi zisizo za kiserikali pamoja na mashirika na kampuni binafsi kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika kufanikisha maadhimisho ya sherehe za
kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Hizi ni sherehe zetu. Kwa hivyo, huu ni wakati mzuri wa kuonesha umoja na mshikamano wetu nchini. Tuzingatie usemi usemao; ‘Mtu lake, hawezi kumwachia mwenzake’ Kwa hivyo, na sisi shughuli hii ni yetu, inahitaji kila mmoja wetu ashiriki. Namuomba kila mmoja wetu auone wajibu huo na ajipange katika kuutekeleza kwa moyo thabiti na uzalendo ili kufanikisha sherehe zetu hizi.
Ndugu Wananchi,
Leo tarehe 15.8.2013 nachukua fursa hii kutamka kwamba Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yamezinduliwa rasmi. Nakutakieni nyote ushiriki na maandalizi mema.
“Tuimarishe Amani, Umoja na Maendeleo – Mapinduzi Daima”.
Ahsanteni
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Pili  wa Rais, Zanzibar

No comments:

Post a Comment