Ndugu
Wananchi;
Kwanza kabisa napenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujaalia amani, umoja, mshikamano na
utulivu, jambo ambalo linazidi kutusaidia katika kupiga hatua za maendeleo ya
kijamii na uchumi katika nchi yetu.
Kama sote tunavyoelewa, nchi
yetu hivi sasa imo katika shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar. Mapinduzi ya Januari 1964 ni mapinduzi yaliyoikomboa nchi
yetu kutoka katika mikono ya kikoloni na kujenga usawa wa wananchi wote bila ya
kujali tofauti zao za kikabila, rangi, imani za dini na mahala wanakotoka.
Aidha, Mapinduzi yameweza nchi yetu kupiga hatua za haraka katika maendeleo ya
kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Sote kwa pamoja tunashuhudia na
kufaidika na matunda ya Mapinduzi, hivyo katika kuadhimisha kutimia miaka 50 ya
Mapinduzi, wananchi wote tunawajibu wa kushiriki kikamilifu katika maandalizi
na kuadhimisha siku hii adhim kwetu.
Katika maadhimisho ya Sherehe
zetu hizi, Serikali imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa Mnara
Maalum wa Kumbukumbu ya Kutimiza Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mnara huu utajengwa
katika eneo la Michenzani, mbele ya nyumba nambari 2 pembeni mwa Maskani ya
Kisonge
Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka
50 ya Mapinduzi utakuwa ni kielelezo (landmark) cha nchi yetu na unakusudiwa
kuwa ni moja ya vivutio vya utalii na sehemu ya kusoma historia ya Mapinduzi. Serikali
ina azma ya kuliendeleza eneo la Michezani kuwa eneo la kisasa kwa kuweka
bustani ya kisasa, kuimarisha miundombinu ya barabara, maegesho ya magari na
maduka ya biashara.
Ujenzi wa minara kama hii si
jambo geni duniani, tumeshuhudia kujengwa kwa minara maarufu kama mnara ulioko Paris,
Ufaranza; Shangai, China na mingine mingi ambayo Miji na Nchi iliyopo minara
hiyo hujipatia umaarufu na hivyo kuvutia watu wa mataifa mbalimbali kwenda
makusudi kuitembelea.
Eneo la Michenzani
limechaguliwa kutokana na historia ya eneo hilo ambalo linaushahidi wa wazi wa
matunda ya mapinduzi. Miongoni mwa matunda hayo ni kuwepo kwa nyumba za
maendeleo na bara bara za kisasa zilizojengwa mara tu baada ya Mapinduzi.
Ujenzi wa Mnara katika eneo
hili la Michezani utafungua njia kwa shughuli nyengine za kimaendeleo na hivyo kuleta haiba nzuri ya eneo hilo na
Mji wa Zanzibar kwa ujumla. Aidha, kuimarika kwa eneo la Michenzani kutatoa
fursa kwa Wananchi walio wengi kujiajiri kutokana na kufanya biashara katika
eneo hilo na kupungunza mrundikano wa watu katika eneo la Darajani.
Tunaelewa kuwa eneo
litakalojengwa mnara huo tayari wananchi wenzetu walikuwa wanalitumia kwa
shughuli mbalimbali. Tunawaomba wananchi wote kuelewa kuwa eneo hilo sasa limo
katika harakati za ujenzi na tunawaomba kutoa ushirikiano kwa kuondoka katika
maeneo hayo ili kupisha shughuli ya kimaendeleo na kihistoria katika nchi yetu.
Kabla ya kumalizia naomba
nichukue fursa hii kuwaomba wananchi wote kushiriki katika shughuli mbali mbali
za maadhimisho katika maeneo yetu. Na pia nawaomba Taasisi za Serikali na Sekta
Binafsi, na Wajasiriamali kujitayarisha vyema kushiriki katika Maonyesho ya
aina yake yatakayofanyika katika Viwanja vy Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Kampasi
ya Beit El Raas. Katika Maonyesho haya
Taasisi mbali mbali zitaonyesha mafanikio ya Taasisi zao katika kipindi cha
miaka 50 iliyopita.
“Tudumishe
Amani, Umoja na Maendeleo ambayo ni Matunda ya Mapinduzi yetu – Mapinduzi Daima”
Ahsanteni
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar
No comments:
Post a Comment