Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ni jambo la
kujivunia kuona, wakati huu Zanzibar ikiadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi
Matukufu ya mwaka 1964, vijana wako mstari wa mbele kuyafurahia,
kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi hayo.Dk. Shein ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza
katika hafla ya kupokea michango kwa ajili ya kuchangia matembezi ya
vijana kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yanayoandaliwa na
Umoja wa Vijana wa CCM–UVCCM Zanzibar.
Katika hafla hiyo ambayo iliyofanyika katika Bwalo la
Maafisa wa Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na
Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali iddi jumla ya shilingi milioni
100 zilikusanywa zikiwa ni ahadi na fedha taslim kati ya shilingi
milioni 150 zilizokusudiwa.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi alichangia jumla ya shilingi milioni 6 na mke wake Mama
Mwanamwema Shein alichangia shilingi milioni 5. Kwa upande wake,Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na marafiki zake alichangia jumla ya shilingi milioni 10.Dk. Shein aliueleza uamuzi huo wa UVCCM Zanzibar kuandaa matembezi hayo ambayo yatafanyika katika mikoa yote mitano ya Zanzibar ni kielelezo cha namna vijana hao wanavyothamini,kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi ya mwaka 1964 ambayo yaliwapa madaraka yakujitawala wenyewe wananchi wa Zanzibar.
Ameusifu uongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM kwa kuandaa matembezi hayo na kueleza kuwa kwa kufanya hivyo wamefuata nyayo za vijana wenzao wa Chama cha Afro Shirazi ambao chini ya uongozi shupavu wa Jemedari wao Mzee Abeid Amani Karume walifanya Mapinduzi tarehe 12 Januari,1960 na kuwakomboa wananchi wa Zanzibar kutoka kwenye ukoloni.
“kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 ni jambo kubwa katika nchi yetu na kwa maendeleo ya watu wetu”alieleza Dk. Shein.Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Matembezi hayo Ndugu Machano Othman Said alisema kuwa matembezi hayo yanatarajiwa kuzinduliwa huko Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi tarehe 22 Disemba, 2013 na kuhitimishwa tarehe 5 Januari, 2014 katika viwanja vya Maisara mjini Unguja ambapo mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Alieleza kuwa lengo la matembezi hayo ambayo yatajumuisha pia vijana kutoka Tanzania Bara ni kutoa hamasa kwa wanachama wa UVCCM na wananchi kwa jumla katika sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba kuhusu Mapinduzi ya mwaka 1964 na ambapo vijana watashiriki pia katika shughuli za kijamii.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM-Taifa Sadifa Juma Khamis aliwashukuru washiriki wote wa hafla hiyo na wale ambao hawakuhudhuria lakini wamewasilisha michango yao kwa kuitikia wito wa kuchangia matembezi hayo.Aidha amemshukuru Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kwa kuwaunga mkono na kuwapa moyo katika maandalizi ya matembezi hayo.
Hafla hiyo imehudhuriwa wa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa CCM na wakereketwa wa chama hicho wakiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Ramadhani Madabida na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka Abdu Shaka.
No comments:
Post a Comment