Sunday, December 15, 2013

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi,akitoa tamko lake la kuichangia Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM,(UVCCM)

Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM,(UVCCM) katika hafla ya Harambee kufanikisha matembezi katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,iliyofanyika leo katika Bwalo la Maafisa wa Polisi,Oysterbay Jijini Dar es Salaam,(kulia) Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Tunajivunia kuona Vijana wanafurahia kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi matukufu ya Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ni jambo la kujivunia kuona, wakati huu Zanzibar ikiadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964, vijana wako mstari wa mbele kuyafurahia, kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi hayo.Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza katika hafla ya kupokea michango kwa ajili ya kuchangia matembezi ya vijana kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yanayoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM–UVCCM Zanzibar.
Katika hafla hiyo ambayo iliyofanyika katika Bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali iddi jumla ya shilingi milioni 100 zilikusanywa zikiwa ni ahadi na fedha taslim kati ya shilingi milioni 150 zilizokusudiwa.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alichangia jumla ya shilingi milioni 6 na mke wake Mama Mwanamwema Shein alichangia shilingi milioni 5. 
Kwa upande wake,Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na marafiki zake alichangia jumla ya shilingi milioni 10.Dk. Shein aliueleza uamuzi huo wa UVCCM Zanzibar kuandaa matembezi hayo ambayo yatafanyika katika mikoa yote mitano ya Zanzibar ni kielelezo cha namna vijana hao wanavyothamini,kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi ya mwaka 1964 ambayo yaliwapa madaraka yakujitawala wenyewe wananchi wa Zanzibar.
Ameusifu uongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM kwa kuandaa matembezi hayo na kueleza kuwa kwa kufanya hivyo wamefuata nyayo za vijana wenzao wa Chama cha Afro Shirazi ambao chini ya uongozi shupavu wa Jemedari wao Mzee Abeid Amani Karume walifanya Mapinduzi tarehe 12 Januari,1960 na kuwakomboa wananchi wa Zanzibar kutoka kwenye ukoloni. 
“kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 ni jambo kubwa katika nchi yetu na kwa maendeleo ya watu wetu”alieleza Dk. Shein.Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Matembezi hayo Ndugu Machano Othman Said alisema kuwa matembezi hayo yanatarajiwa kuzinduliwa huko Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi tarehe 22 Disemba, 2013 na kuhitimishwa tarehe 5 Januari, 2014 katika viwanja vya Maisara mjini Unguja ambapo mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. 
Alieleza kuwa lengo la matembezi hayo ambayo yatajumuisha pia vijana kutoka Tanzania Bara ni kutoa hamasa kwa wanachama wa UVCCM na wananchi kwa jumla katika sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba kuhusu Mapinduzi ya mwaka 1964 na ambapo vijana watashiriki pia katika shughuli za kijamii.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM-Taifa Sadifa Juma Khamis aliwashukuru washiriki wote wa hafla hiyo na wale ambao hawakuhudhuria lakini wamewasilisha michango yao kwa kuitikia wito wa kuchangia matembezi hayo.Aidha amemshukuru Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kwa kuwaunga mkono na kuwapa moyo katika maandalizi ya matembezi hayo. 
Hafla hiyo imehudhuriwa wa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa CCM na wakereketwa wa chama hicho wakiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Ramadhani Madabida na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka Abdu Shaka.

Sunday, October 27, 2013

MNARA WA KUMBUKUMBU WA MIAKA 50 YA MAPINDUZI ZANZIBAR

MUONEKANO WA MNARA WA KUMBUKUMBU YA SHEREHE YA MIAKA 50 YA MAPINDUZI ZANZIBAR UNAOJENGWA HAPO MICHEZANI KARIBU NA MASKANI YA KISONGE

Tuesday, October 15, 2013

Risala ya Mhe:Rais wa Zanzibar na MBLM,kwa ajili ya uzinduzi wa sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi.


Ndugu Wananchi,
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mara nyengine kwa kutujaalia kufunga na kukamilisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na tukaweza kusherehekea Sikukuu ya Idd el Fitri kwa furaha, amani na utulivu. Namuomba Mwenyezi Mungu (SW) azikubali ibada zetu na atuzidishie amani, utulivu na kila lenye kheri katika nchi yetu. Kama tunavyoelewa, kila ifikapo tarehe 12 Januari ya kila mwaka, nchi yetuhuadhimisha Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.Mapinduzi haya ambayo yaliongozwa na Jemedari wetu Mkuu, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ndiyo yaliyowakomboa wananchi wa Zanzibar kwa kuondoa utawala wa kigeni, ubaguzi wa watu na kuweka usawa katika jamii ya Wazanzibari. Hivyo, ni wazi kuwa Mapinduzi haya ndiyo msingi wa uhuru, usawa na maendeleo katika nchi yetu hadi tulipofikia.

Miezi mitano ijayo, yaani ifikapo tarehe 12 Januari, 2014, Mapinduzi yetu yatakuwa yamefikia miaka 50 sawa na nusu karne. Bila ya shaka, nusu karne hii ya Mapinduzi inatufikia wakati nchi yetu ikiwa imepiga hatua kubwa za kimaendeleo na kuimarika kwa hali ya amani, utulivu, umoja na mshikamano. Kutokana na hali hiyo, ni dhahiri kuwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuadhimisha kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi yetu kwa sherehe za aina yake, zenye hadhi na haiba inayolingana na mafanikio ya maendeleo tuliyofikia.

Ndugu Wananchi,
Sherehe zetu hizi zinakwenda na kauli mbiu isemayo “Tuimarishe Amani, Umoja na Maendeleo – Mapinduzi Daima”. Kauli mbiu hii inatushajiisha wananchi wote
kujivunia Amani tuliyonayo, Umoja tulionao na hatua kubwa ya Maendeleo tuliyofikia. Jambo la msingi kabisa ni kuilinda amani hiyo, kudumisha umoja wetu na pia kuthamini, kuyaenzi na kuyaimarisha maendeleo yetu. Ni vyema tukatambua kuwa mambo hayo ndiyo hazina muhimu kwa mustakbali mwema wa Wazanzibari na Watanzania wote tuliopo na wale watakaokuja baada ya sisi.
Ndugu Wananchi,
Katika kuadhimisha Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi yetu Matukufu, Serikali imepanga kufanya mambo mbali mbali katika kipindi hiki cha miezi mitano kabla ya kufikia kilele hapo tarehe 12 Januari, 2014 katika Uwanja wa Amaan. Serikali imetoa muongozo wa namna sherehe hizi zitakavyofanyika katika maeneo mbali mbali ya visiwa vyetu vya Unguja na Pemba kwa shamra shamra na mvuto wa kipekee. Bila ya shaka, sote tuna wajibu wa kufuata maelekezo yaliyomo katika muongozo huo na yale yatakayokuwa yanatolewa na viongozi wetu kila mara ili sherehe zetu zifanyike kwa utaratibu maalum wenye kupendeza na usiokuwa na bughudha.
Ndugu Wananchi,
Ni vyema tukaelewa kuwa sherehe hizi ni za kila mmoja wetu, si za Serikali peke yake wala si za chama fulani; ni za kila mwananchi awe mmoja mmoja au kwa makundi. Kila mtu ana wajibu na haki ya kushiriki katika shamra shamra za sherehe hizi kwa namna utaratibu utakavyoelekeza.

Ni dhahiri kuwa matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya kipindi hiki cha miaka 50 yanabainika waziwazi katika kila sekta na nyanja za maisha yetu iwe ni serikalini au ndani ya jamii katika maeneo tunamoishi. Tunapaswa kujivunia na kuyathamini mafanikio hayo ya Mapinduzi nchini kwa vitendo. Hatua kubwa ya maendeleo tuliyofikia ni ithibati na kielelezo muhimu cha ufanisi kwa wale wote wanaoikumbuka
Zanzibar ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964. Sote tuna jukumu la kuyaimarisha maendeleo hayo na kudumisha hali ya amani na umoja wetu. Napenda kutoa wito kwenu wananchi nyote, taasisi za serikali ambazo tayari
zimeshaelekezwa, taasisi zisizo za kiserikali pamoja na mashirika na kampuni binafsi kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika kufanikisha maadhimisho ya sherehe za
kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Hizi ni sherehe zetu. Kwa hivyo, huu ni wakati mzuri wa kuonesha umoja na mshikamano wetu nchini. Tuzingatie usemi usemao; ‘Mtu lake, hawezi kumwachia mwenzake’ Kwa hivyo, na sisi shughuli hii ni yetu, inahitaji kila mmoja wetu ashiriki. Namuomba kila mmoja wetu auone wajibu huo na ajipange katika kuutekeleza kwa moyo thabiti na uzalendo ili kufanikisha sherehe zetu hizi.
Ndugu Wananchi,
Leo tarehe 15.8.2013 nachukua fursa hii kutamka kwamba Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yamezinduliwa rasmi. Nakutakieni nyote ushiriki na maandalizi mema.
“Tuimarishe Amani, Umoja na Maendeleo – Mapinduzi Daima”.
Ahsanteni
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Pili  wa Rais, Zanzibar

Thursday, October 10, 2013

TAARIFA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS MHESHIMIWA MOHAMED ABOUD MOHAMED KUHUSU UJENZI WA MNARA WA KUMBUKUMBU YA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR


Ndugu Wananchi;

Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujaalia amani, umoja, mshikamano na utulivu, jambo ambalo linazidi kutusaidia katika kupiga hatua za maendeleo ya kijamii na uchumi katika nchi yetu.

 Kama sote tunavyoelewa, nchi yetu hivi sasa imo katika shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Mapinduzi ya Januari 1964 ni mapinduzi yaliyoikomboa nchi yetu kutoka katika mikono ya kikoloni na kujenga usawa wa wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za kikabila, rangi, imani za dini na mahala wanakotoka. Aidha, Mapinduzi yameweza nchi yetu kupiga hatua za haraka katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Sote kwa pamoja tunashuhudia na kufaidika na matunda ya Mapinduzi, hivyo katika kuadhimisha kutimia miaka 50 ya Mapinduzi, wananchi wote tunawajibu wa kushiriki kikamilifu katika maandalizi na kuadhimisha siku hii adhim kwetu.
 Katika maadhimisho ya Sherehe zetu hizi, Serikali imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa Mnara Maalum wa Kumbukumbu ya Kutimiza Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mnara huu utajengwa katika eneo la Michenzani, mbele ya nyumba nambari 2 pembeni mwa Maskani ya Kisonge
Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi utakuwa ni kielelezo (landmark) cha nchi yetu na unakusudiwa kuwa ni moja ya vivutio vya utalii na sehemu ya kusoma historia ya Mapinduzi. Serikali ina azma ya kuliendeleza eneo la Michezani kuwa eneo la kisasa kwa kuweka bustani ya kisasa, kuimarisha miundombinu ya barabara, maegesho ya magari na maduka ya biashara.

Ujenzi wa minara kama hii si jambo geni duniani, tumeshuhudia kujengwa kwa minara maarufu kama mnara ulioko Paris, Ufaranza; Shangai, China na mingine mingi ambayo Miji na Nchi iliyopo minara hiyo hujipatia umaarufu na hivyo kuvutia watu wa mataifa mbalimbali kwenda makusudi kuitembelea.
Eneo la Michenzani limechaguliwa kutokana na historia ya eneo hilo ambalo linaushahidi wa wazi wa matunda ya mapinduzi. Miongoni mwa matunda hayo ni kuwepo kwa nyumba za maendeleo na bara bara za kisasa zilizojengwa mara tu baada ya Mapinduzi.


Ujenzi wa Mnara katika eneo hili la Michezani utafungua njia kwa shughuli nyengine za kimaendeleo na hivyo kuleta haiba nzuri ya eneo hilo na Mji wa Zanzibar kwa ujumla. Aidha, kuimarika kwa eneo la Michenzani kutatoa fursa kwa Wananchi walio wengi kujiajiri kutokana na kufanya biashara katika eneo hilo na kupungunza mrundikano wa watu katika eneo la Darajani.

Tunaelewa kuwa eneo litakalojengwa mnara huo tayari wananchi wenzetu walikuwa wanalitumia kwa shughuli mbalimbali. Tunawaomba wananchi wote kuelewa kuwa eneo hilo sasa limo katika harakati za ujenzi na tunawaomba kutoa ushirikiano kwa kuondoka katika maeneo hayo ili kupisha shughuli ya kimaendeleo na kihistoria katika nchi yetu.
Kabla ya kumalizia naomba nichukue fursa hii kuwaomba wananchi wote kushiriki katika shughuli mbali mbali za maadhimisho katika maeneo yetu. Na pia nawaomba Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi, na Wajasiriamali kujitayarisha vyema kushiriki katika Maonyesho ya aina yake yatakayofanyika katika Viwanja vy Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Kampasi ya Beit El Raas.  Katika Maonyesho haya Taasisi mbali mbali zitaonyesha mafanikio ya Taasisi zao katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

 

“Tudumishe Amani, Umoja na Maendeleo ambayo ni Matunda ya Mapinduzi yetu – Mapinduzi Daima”

Ahsanteni
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Pili  wa Rais, Zanzibar